UCHANGANUZI WA MITAZAMO YA KIIMANI NA KISEKULA KUHUSU LUGHA

YASIN S. MUSA, BADRU M. HAROON, NAWAJE A. MGANGA

ABSTRACT


Lugha ni nyenzo ya kipekee katika mawasiliano ya viumbe vyote. Kwa karne nyingi dhana ya lugha imeibua mijadala mingi kiasi cha kuwafanya wanaisimu kubaki njia panda kutokana na kukosa mwafaka kuhusu maana na chanzo cha lugha. Ingawa kuna imani tofauti katika uso wa dunia hii, lakini imani zenye wafuasi wengi ni Ukristo na Uislamu. Kwa mnasaba wa makala hii, mtazamo wa kiimani utakaorejelewa ni imani ya Kiislamu, na hizo imani nyengine zitadokezwa tu itakapobidi. Mathalan, Usekula ni imani isiyojinasibisha na maswala ya kidini katika maendeleo ya jamii kupitia nyanja zote za kimaisha. Wasekula hawaamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo ndani yake; akiwemo mwanadamu na lugha, bali huamini kuwa vimetokea kwa bahati nasibu tu; na kwa hivyo vitatoweka pasi na utaratibu mahsusi. Ukristo hueleza kuwa lugha ni zawadi kutoka kwa Mungu wa Adamu; ndiye aliyevipa vitu vyote majina. Vivyo hivyo, unashikilia kuwa tofauti ya ndimi chanzo chake ni utengano uliojitokeza baada ya mnara wa Babeli kuanguka na watu waliokuwa wanaupanda kutapakaa sehemu mbalimbali. Uislamu ni dini inayoamini kwamba asili na chanzo cha lugha ni Mwenyezi Mungu. Ni neema ya Mwenyezi Mungu[1] kwa viumbe wake katika mawasiliano ili wapate kulifikia vyema lengo la kuumbwa kwao. Kwa mantiki hiyo, mjadala wa makala  hii umeiangalia lugha kwa mtazamo wa Kiislamu kama inavyoelezewa katika mafundisho yake,



[1] Mwenyezi Mungu anayekusudiwa au anayeaminiwa na Waislamu, ambaye kwa itikadi yao ndiye muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo anaitwa Allah kwa Kiarabu.